Mashirika mbalimbali ya ndege duniani yamekwepa anga za Iran na Iraq kufuatia mzozo wa Marekani na Iran.
Kufuatia shambulio la kombora la Iran dhidi ya kambi za kijeshi ambapo vikosi vya jeshi la Marekani na vikosi vya muungano viliweka kambi, mashirika kadhaa ya ndege yamebadili njia zao kutoka anga la Iran na Iraq.
Mara baada ya shambulio hilo, Mamlaka za usafirishaji wa anga nchini Marekani zilitangaza kuzuia mashirika yake kupita katika anga za Iraq, Iran, Ghuba ya Oman na bahari kati ya Iran na Saudi Arabia.
Kando na Marekani, mashirika kadhaa ya ndege ya Asia na Ulaya pia yameeleza kuepuka anga la Iran.
Wakala wa habari nchini India, Asian News International (ANI), lilinukuu vyanzo vya serikali kwamba mashirika yote ya ndege ya India yametakiwa kuepuka anga za Iran, Iraqi na Ghuba kufuatia mvutano katika eneo hilo.
Shirika la ndege la Singapore (Singapore Airlines) pia limebadili njia zake kukwepa anga la Iran.
"Kwa kuzingatia yanayoendelea kati ya Amerika na Iran, ndege zote za Singapore Airlines ndani na nje ya Ulaya zinaelekezwa kuepuka anga la Iran," shirika hilo lilisema.
"Tunafuatilia hali hiyo kwa karibu na tutafanya marekebisho sahihi kwa njia zetu ikiwa ni lazima," liliongeza.
Shirika kubwa zaidi la usafiri wa anga nchini Taiwan, China Airlines ilisema katika taarifa kwamba itaendelea kuangalia hali inavyokwenda na kisha kurekebisha njia ipasavyo, liliripoti Reuters.
Shirika lingine la Taiwan, EVA Air, na Malaysia Airlines pia yamesema wanaepuka kuruka juu ya anga la Iran.
Shirika la Korean Air limesema lilikuwa likiepuka anga la Iran na Iraq kabla ya shambulio dhidi ya kambi za Marekani.
Shirika la Australia, Qantas, limesema lilibadilisha njia yake ya London kwenda Perth, Australia, kuepuka anga za Iran na Iraq hadi taarifa zaidi zitakapotolewa, limeripoti Associated Press.
Wakala wa anga wa Urusi, Rosaviatsia, pia limetoa pendekezo rasmi kwa mashirika yote ya ndege ya Urusi kujiepusha kuruka juu ya Iran, Iraqi, Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman "kutokana na hatari zilizopo kwa usalama wa ndege za kimataifa."
Shirika la ndege la Ujerumani, Lufthansa, limefuta safari yake kutoka Frankfurt kwenda Tehran Jumatano kwa kuzingatia hali ya sasa, limeripoti Associated Press.
Shirika la ndege la Ufaransa Air France lilisema kampuni hiyo imesimamisha safari zake juu ya anga la Iraq na Iran, limeripoti Reuters.
"Mipango ya ndege itarekebishwa kwa wakati kulingana na maamuzi ya viongozi wa Ufaransa na wa kikanda, ili kuhakikisha kiwango cha juu cha usalama wa ndege", Air France ilisema katika taarifa yake
Shirika linalomilikiwa na Falme za Kiarabu (UAE), Flydubai, limefuta safari iliyopangwa Jumatano kutoka Dubai kwenda Baghdad, lakini likiendelea safari kwenda Basra na Najaf.
Safari za shirika la Emirates kati ya Dubai na Baghdad zimefutwa.
No comments:
Post a Comment